Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Wananchi waaswa kutunza miradi ya TASAF


Wakazi wa Shehia ya Kinyikani na maeneo jirani katika wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, wametakiwa kutunza miundombinu ya kituo cha Afya  Kinyikani kilichojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF, ili kidumu kwa muda mrefu na kutoa huduma kwa wananchi.

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kusini Pemba Amour Hamad Saleh wakati wa utoaji wa vyeti vya  pongezi kwa wajumbe wa kamati za usimamizi wa jamii walioshiriki katika mchakato  wote wa ujenzi wa kituo hicho.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mkoa wa Kusini Pemba Amour Hamad Saleh akizungumza  wakati wa tukio la kukabidhi vyeti kwa Wasimamizi wa kamati za usimamizi wa Jamii walioshiriki kwenye ujenzi wa  Kituo cha Afya Kinyikani katika wilaya ya Wete  Mkoa wa Kaskazini Pemba, Visiwani Zanzibar

Ujenzi wa kituo hicho umegharimu jumla ya shilingi milioni 552 ambazo zimejumuisha majengo ya kutolea huduma muhimu kwa wagonjwa wa nje, jengo la huduma mama na mtoto, pamoja na nyumba mbili za ya watumishi.

“Kituo hiki ni muhumu sana kwani kimerahisisha upatikaaji wa huduma bora za afya ambazo hapo awali hazikuwepo katika shehia hii na maeneo jirani,” alisema na kuongeza kuwa, ni muhumu kwa wananchi pamoja na kamati ya usimamizi wa jamii kuendelea kulinda miundombinu hiyo ili kuwe na tija ya muda mrefu.

Mkurugenzi wa Uratibu kutoka TASAF Bi. Haika Shayo akizungumza wakati wa tukio la kukabidhi vyeti kwa Wasimamizi wa kamati za usimamizi wa Jamii walioshiriki kwenye ujenzi wa  Kituo cha Afya Kinyikani katika wilaya ya Wete  Mkoa wa Kaskazini Pemba,Visiwani Zanzibar

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Shedrack Mziray, Mkurugenzi wa Uratibu wa TASAF Haika Shayo alisema TASAF inaendeleza juhudi za Serikali katika kupunguza umaskini kwa kaya zenye upungufu wa mahitaji ya msingi ili kuziwezesha kaya hizo zenye hali duni kiuchumi kuongeza kipato, fursa za kiuchumi na uwezo wa kugharimia mahitaji muhimu ya kila siku na kujenga rasilimali watu.

“Mfuko huu unasaidia kujenga miundombinu kwenye Jamii zenye upungufu kwa sekta za Elimu, Afya, Barabara vijijini au za kijamii ili kuwezesha upatikanaji wa huduma hizo kwa urahisi,” alisema.

Katika kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wananchi Zanzibar katika kipindi cha Pili cha Mpango TASAF imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi 15 ya kuendeleza miundombinu katika sekta ya Elimu, Afya na Maji. Miradi hiyo imegharimu zaidi ya Shillingi za kitanzani Bilioni 3.1.

“Kwa mwaka wa fedha 2023/24, katika Mamlaka ya Eneo la Utekelezaji Pemba, TASAF inatekeleza jumla ya miradi saba ya miundo mbinu yenye thamani ya zaidi ya Shilingi za kitanzania Bilioni 1.32. Miradi hiyo inahusisha sekta tofauti ikiwemo afya ambayo miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kinyikani ambacho kimekamilika na kuanza kutoa huduma,” aliongeza.

Kwa upande wake, Katibu wa Kamati ya Wasimamizi wa Jamii Amour Khamis Amour aliishukuru Serikali kupitia TASAF kwa kutekeleza miradi ya inayosaidia urahisi katika upatikanaji wa huduma za kijamii.

“Mradi huu una umuhimu sana kwetu, tutaendelea kuutunza kwa manufaa ya sasa na baadaye,” alisema.