Habari
Wanufaika wa TASAF wahamasika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi

Mtaalam wa mabadiliko ya tabia nchi kutoka Benki ya Dunia Bw Marco Alcaraz akiwasilisha mada ya mabadiliko ya tabia nchi
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF kwa kushirikiana na Benki ya Dunia na Wakala wa Maendeleo wa Norway wameendesha mafunzo kwa washiriki 50 wakiwemo wakuu wa Idara, Wataalamu wa sekta na Wawezeshaji wa shughuli za TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kuhusu mabadiliko ya tabia nchi. Washiriki hao waliweza uzoefu wao kuhusu mabadiliko ya tabia nchi kwenye maeneo wanayotoka baada ya kupata mawasilisho kutoka kwa Mtaalam wa Mabadiliko ya Tabia Nchi wa Benki ya Dunia Bw Marco Alcaraz.
Ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, wawezeshaji hao wamesema wamepanda mazao ya chakula na biashara yanayohimili ukame, mazao yanayorutubisha udongo na kuzuia mmomonyoko wa ardhi, kuchimba makinga maji na malambo ya kuhifadhia maji na kuanzisha kilimo cha matuta ya nusu duara kwa ajili ya kuhifadhi maji kwenye maeneo ya miinuko miradi ya ajira za muda kwa walengwa.
Baada ya mafunzo wataalamu kutoka TASAF Makao Makuu, Benki ya Dunia na Wakala wa Maendeleo kutoka Norway walitembelea vijiji vya Handali, Chihembe, Muungano, Mjeloo na Chanhumba kuona namna walengwa wa maeneo hayo wanavyokabiliana na suala la mabadiliko ya tabia nchi. Timu hiyo ya wataalam ilikutana na Viongozi wa Vijiji pamoja na baadhi ya wanufaika na kubadilishana uzoefu.
Wataalamu kutoka TASAF Makao Makuu, Benki ya Dunia na Wakala wa Maendeleo wa kutoka Norway kwenye mkutano na wananchi
Katika kijiji cha Handali, walengwa wanakabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kulima mahindi, mtama na alizeti kwa njia ya matuta ya nusu duara ili kuhifadhi maji kwenye maeneo ya miinuko. Kupitia kilimo hicho cha matuta ya nusu duara wameongeza mavuno kutoka gunia la mahindi, na robo tatu ya gunia la mtama kwa heka hadi kufikia gunia 3 za mahindi na mtama na gunia mbili za alizeti kwa heka moja. Ili kuhifadhi maji kwa ajili ya matumizi mbali mbali kama kunywesha mifugo, umwagiliaji na matumizi mengine ya nyumbani, walengwa wamechimba mabwawa, malambo na makinga maji.
Katika Kijiji cha Chihembe walengwa wameanzisha lambo la kudumu linalowapa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, mifugo na shughuli zingine za nyumbani. Aidha wamejenga kinga maji ambalo linazuia mafuriko wakati wa msimu wa mvua. Eneo hilo sasa ni la kijani muda wote na shughuli kubwa inayofanyika ni kilimo cha mbogamboga ambacho kinainua kipato kwa wanakaya wa Kijiji hicho.
Ujenzi wa barabara na bwawa la umwagiliaji umefanyika katika Kijiji cha Muungano kupitia Miradi ya Ajira za Muda. Barabara iliyojengwa imerahisisha usafirishaji wa mazao kutoka shambani hadi kwenye masoko na bwawa linatoa maji kwa ajili ya mifugo, kilimo na matumizi ya nyumbani.
Visima vya maji, barabara na kilimo cha mazao yasiyotegemea mvua nyingi kama Korosho na mtama kimeanzishwa katika Kijiji cha Mjeroo. Shughuli hizi mbali na kuongeza kipato zimetoa mchango mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Katika Kijiji cha Chanhumbe walengwa wamejenga makinga maji, barabara na upandaji miti ambao umeongeza eneo kwa ajili ya kivuli na kukinga upepo mkali uliokuwa unaathiri maeneo mbali mbali ya Kijiji ikiwemo eneo la shule na ujenzi wa makinga maji umeimarisha upatikanaji wa maji.
Baada ya kutembelea miradi yote hiyo, Mtalamu wa Kilimo kutoka Norway ambaye pia ni mkulima, alionyesha athari inavyotokea kwenye ardhi isiyo na majani inaponyeshewa na mvua na alielekeza jinsi ya kupanda mbegu na kustawisha mazao kwa miaka mingi kwa kuchimba mashimo na kuweka mbolea kwa ajili ya msimu ujao wa kilimo. Kilimo hicho hurahisisha mkulima kupanda mbegu bila kulima eneo kubwa la shamba
Bw Odd Eirik Amesen akionyesha mfano wa jinsi maji ya mvua yanavyopotea kirahisi kwenye ardhi isiyokuwa na majani hata makavu wakati wa kiangazi
Bw. Odd Eirik Amesen akionyesha mfano wa jinsi ya kuchimba mashimo kwa ajili ya kupanda mbegu bila kulima eneo kubwa