Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Washirika wa Maendeleo wa TASAF Wawapongeza Wanawake kwa Uongozi Bora Iringa


Mmoja wa Washirika wa Maendeleo Bw. Matthew Cogan kutoka Ubalozi wa Ireland akijibu Maswali ya Wanahabari wakiwa katika Kijiji cha Iramba mara baada ya kukagua Mradi wa Miti katika Kijiji hicho

Washirika wa Maendeleo wa TASAF wamewapongeza Wanawake Mkoani Iringa kwa kufanya vizuri katika nafasi zao za uongozi kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa Miradi ya TASAF kutoka ngazi ya Vijiji/Mitaa hadi Mkoa.

Hayo yalisemwa na Mwakilishi wa Washirika wa Maendeleo kutoka nchi ya Ireland, Bw. Matthew Cogan wakati wa majumuisho ya ziara waliyofanya hivi karibuni Mkoani Iringa ikiwa ni sehemu ya Mapitio ya pamoja ya Utekelezaji Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa baina ya Serikali na Washirika Maendeleo.

Bw. Matthew Cogan aliyasema hayo baada ya kuona kuwa sehemu kubwa ya viongozi katika ngazi ya Mkoa hadi Kijiji ni wanawake na kazi zao zinaonekana kuwa nzuri sana.

“Nimeshangaa kila mahali tunakwenda tunapokewa na wanawake na kazi yao ni nzuri sana. Kwa mfano, Rais wa Tanzania ni Mwanamke, Kiongozi wa Timu toka TASAF (Mkurugenzi wa Uratibu wa TASAF) ni Mwanamke, Mkuu wa Mkoa ni Mwanamke, Mratibu wa TASAF Mkoa ni Mwanamke, Mratibu wa TASAF Wilaya ya Mufindi ni Mwanamke, Mtendaji wa Kijiji cha Ikangamwani ni Mwanamke na Mtendaji wa Kijiji cha Iramba ni Mwanamke. Hii imetufurahisha sana”, alisema Bw. Cogan.

“Wanaume tumeachwa nyuma sana na inatubidi kufanya bidii ili kupata nafasi na kufanya vizuri kama wanawake wanavyofanya”, aliongeza Bw. Cogan.

Timu ya Washirika wa Maendeleo iliyotembelea Mkoa wa Iringa kukagua utekelezaji ya Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa ilijumuisha Maafisa kutoka Ofisi ya Rais- Ikulu, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Wawakilishi kutoka Benki ya Dunia, Ubalozi wa Ireland, pamoja na Watumishi wa TASAF.

Mkurugenzi wa Uratibu na Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF kwa Timu iliyotembelea Mkoa wa Iringa, Bi. Haika Shayo akijibu Maswali ya Wanahabari (hawako pichani) katika Kijiji cha Iramba mara baada ya kukagua Mradi wa Miti katika Kijiji hicho

Washirika wa Maendeleo wanaofadhili Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa unaotekelezwa na TASAF hukutana na Serikali kila baada ya miezi sita kupitia kwa pamoja Utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa ikiwa ni pamoja na kutembelea maeneo ya Utekelezaji kuona utekelezaji wa Mpango hadi ngazi ya jamii. ili kutoa maoni na ushauri kwa nia ya kuboresha utendaji na kuleta tija kwa Mpango.

Ujumbe wa ziara hiyo umefurahishwa na utekelezaji wa Mpango na kuona kuwa Mpango unafahamika vizuri kwa walengwa,  na pia taarifa walizopokea kuhusu utekelezaji wa Mpango zimeendana na uhalisia uliopo.

Mratibu wa TASAF wa Mkoa wa Iringa, Bi. Saida Mgeni (aliyesimama) akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa TASAF ya Mkoa wa Iringa wakati Timu ya Wadau wa Maendeleo walipofika Mkoani hapo wakiwa kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa TASAF

Wananchi wa Kijiji cha Ikangamwani wakicheza kufurahia Ugeni wa Washirika wa Maendeleo wa TASAF ulioambatana na Timu kutoka TASAF walipofika Kijijini hapo kukagua Miradi

Timu ya Washirika wa Maendeleo wakiwa nyumbani kwa Bi. Shani William Mkonda (hayuko pichani) wakimsikiliza namna anavyopambana kuondokana na umaskini

Mtendaji wa Kijiji cha Iramba Bi. Mtono akisoma taarifa ya Utekelezaji wa Mpango wa TASAF kwa Timu ya Washirika wa Maendeleo walipofika kukagua Miradi ya TASAF Kijijini hapo