Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Washiriki wa Mkutano wa Mapitio ya Pamoja ya Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa wakamilisha ziara Mkoa wa Kilimanjaro


Kiongozi wa Shughuli za TASAF kutoka Benki ya Dunia Bi. Claudia Zambra Taibo amepongeza mchango wa Serikali kwenye utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa mkoani Kilimanjaro ikiwemo kukamilika kwa miradi na kuboresha maisha ya wanufaika.

Mwakilishi huyo wa Benki ya dunia ametoa pongezi hizo katika kikao cha majumuisho ya ziara ya washiriki wa Mkutano wa Mapitio ya pamoja  ya utekelezaji wa mpango wa kunusuru wa kaya za walengwa unaotekelezwa na TASAF katika mkoa wa Kilimanjaro ambapo ameshauri kuwa miradi mingine itakayobuniwa ni vyema wananchi washirikishwe tangu hatua za awali ikiwemo aina ya miradi pendekezwa.

Bi. Claudia Zambra Taibo, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha taratibu za malipo ili kupunguza malalamiko miongoni mwa wanufaika.

'Mpango wa kuhama kutoka malipo ya fedha taslimu kwenda malipo ya mtandao ni mzuri, japo ni vyema kuzitatua changamoto ndogo ndogo zinazojitokeza hususani zinazohusu upatikanaji wa vitambulisho." amesema Claudia Taibo

Pamoja na Benki ya Dunia, Washirika wengine wa Maendeleo walizungumzia ziara ya Mkoa wa Kilimanjaro katika kikao hicho cha majumuisho ni pamoja na Mwakilishi kutoka Serikali ya Canada ambaye ni Mshirika wa Maendeleo

mpya kwenye Mpango wa TASAF, na kwa mujibu wa Mwakilishi huyo, Ndg. Marc Leblanc alisema ziara hiyo imetoa taswira na uzoefu wa utekelezaji wa Mpango.

"Sisi kama washirika wapya wa TASAF, ziara hii imetusaidia kujua jinsi kazi ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa inavyofanyika, zaidi imetufanya kuifikia jamii ya wanufaika, jambo ambalo limetuongezea ufahamu." amesema Marc Leblanc.

Kikao hicho cha majumuisho katika Mkoa wa Kilimanjaro ni sehemu ya maandalizi kwa ajili ya taarifa ya mapitio ya pamoja ya utekelezaji wa Mpango kimeongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Ndg. Tixon Nzunda ambaye kwa niaba ya serikali ameipoongeza timu na kuwashukuru washirika wa maendeleo huku akitoa takwimu za mafanikio yaliyopatikana mkoani Kilimanjaro kupitia Mpango wa TASAF.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Ndugu Tixon Nzunda aliposhiriki Kikao cha Majumuisho Baada ya Kukamilika kwa Ziara ya Washiriki wa Mkutano wa Mapitio ya Pamoja ya Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa katika Mkoa huo

Katibu Tawala ameeleza jinsi Serikali ya Mkoa wa kIlimanjaro inavyoshiriki kuhakikisha Mpango wa Serikali wa Kunusuru Kaya za Walengwa kupitia TASAF unafanikiwa, hususani katika usimamizi wa miradi ya maendeleo inayobuniwa pamoja na kuhakikisha changamoto zinazowakabili wanufaika zinatatuliwa kwa pamoja na kwa haraka.

"Kila mwezi huwa tunakuwa na vikao vya tathmini ya utekelezaji wa miradi mbalimbali kuanzia ngazi za zote za Serikali ya Mkoa, ikiwemo mpango huu wa TASAF, na tunapokea taarifa mbalimbali ikiwemo malalamiko ambayo tunayafanyia kazi." amesema Katibu Tawala Tixon Nzunda

Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa Mapitio ya Pamoja ya Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa Wakiwa Katika Kikao cha Majumuisho 

Washiriki wa Mkutano wa mapitio ya pamoja ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa wamekamilisha ziara yao mkoani Kilimanjaro, ambapo kwa mujibu wa Uongozi wa TASAF, malengo ya Mpango yamepata mafanikio makubwa ikiwemo maboresho ya miradi, ajira za muda, kujenga uwezo kwa walengwa kwenye afua mbalimbali na utoaji wa rukuzu kwa walengwa.