Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Waziri Simbachawene akagua Ujenzi wa Shule inayojengwa na TASAF


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene akiwa katika ziara yake mkoani Geita alitembelea wilayani Chato, ambapo pamoja na masuala mengine ametembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na TASAF.

Mhe. Simbachawene ametembelea miradi miwili ya ujenzi wa shule ya Sekondari na Kituo cha Afya.  Serikali kupitia TASAF imetoa shilingi milioni 749.7 kujenga shule hiyo ambayo unajumuisha ujenzi wa jengo la utawala bweni,madarasa nane kisima cha maji ,matundu 28 ya choo na maabara.

Akitembelea mradi huo Waziri Simbachawene amesema lengo la miradi inayotekelezwea kwa fedha za Tasaf ni kuona inawasaidia wananchi na kubadilisha maeneo yao kutoka kwenye hali ya umaskini na kujikwamua kiuchumi.

Amesema katika kutekeleza ilani ya CCM ya kuwaletea wananchi maisha bora miradi hiyo ndio kipimo cha kuwaletea wananchi maisha bora hivyo wananchi wana wajibu wa kutunza miradi hiyo ili iwe endelevu. 

Ujenzi wa mradi wa shule utaondoa changamoto ya usafiri kwa wanafunzi wanaotoka katika kijiji cha Mkungo kata ya Bukome waliokuwa wanalazimika kutembea umbali wa kati ya kilomita 17 hadi 22 kwenda shule iliyopo kata jirani ya Buzirayombo. Waziri Simbachawene ameziagiza halmashauri kuhakikisha mchango wa asilimia kumi ambao wananchi wanatakiwa kuchangia zitumike kuweka samani kwenye miundombinu hiyo.

‘Miradi hii iwe ya mfano. Ikikamilika iwe na samani, maji na umeme ili wanafunzi wasome kwenye mazingira bora na rafiki” alisema Waziri Simbachawene.

 “Wanafunzi waliokuwa wakitoka maeneo haya walikuwa wakitembea umbali mrefu mwenye uwezo kidogo alitembelea baiskeli lakini wengi walitembea kwa miguu wanafika shule wamechoka hata wakifundishwa hawaelewi mradi huu utasaidia sana kukuza ufaulu kwa wanafunzi” Alisema Mbunge Merald Kalemani.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Chato Mandia Kihiyo amesema TASAF kwa kipindi cha 2021/23 umetekeleza miradi yenye thamani ya Shilingi Bilioni 8.7  na kunufaisha walengwa 9,832 katika vijiji 115 vya halmashauri hiyo.