Habari
Mtandao wa Wabunge wa WB, IMF watembelea miradi ya TASAF Dodoma

Ujumbe wa Mtandao wa Wabunge wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa walipotembelea mradi wa lambo la Chaco katika Kijiji cha Ikombolinga wilayani Chamwino Dodoma
Mwenyekiti wa Mtandao wa Wabunge wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa, (PNoWB) Liam Byrne Ijumaa Septemba 23, 2022 ametembelea miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF katika Kijiji cha Ikombolinga wilayani Chamwino, Dodoma na kukutana na wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa na kutembelea mradi.
Bw. Byrne alifuatana na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni wanachama wa mtandao huo, Mhe. Neema Lugangira, Mhe. Hadija Taya, Mhe. Alice Kaijage na Mhe. Alfred Kimea.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwanachama wa mtandao huo wa Mabunge duniani wenye matawi katika nchi zaidi ya 140 na wanachama zaidi ya 1,000.
Akizungumza na wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa. Bw. Bayrne ambaye pia alipata kuwa Waziri wa Fedha wa Uingereza alisema amafurahishwa na shuhuda za walengwa na atazieleza kwa watu wengine duniani ili na waweze kujifunza kutoka Tanzania.
Mmoja wa walengwa hao, Margaret Puma (68) alieleza maisha yake ya awali kabla hajaingia katika Mpango na kusimulia jinsi alivyoanza kutumia ruzuku yake ya kwanza kwa kukodi shamba na kuanza kilimo cha alizeti ambacho kilimpatia fedha ya kutosha kujenga nyumba ya bati na kununua mifugo.
Margaret ni mmoja kati ya wanufaika 437 katika Kijiji cha Ikombolinga kilichoingizwa kwenye Mpango mwaka 2015.
Ujumbe huo pia ulitembelea lambo lililochimbwa chini ya Mradi wa Ajira za Muda kwa lengo la kumaliza tatizo la maji kwa matumizi ya nyumbani na kunyweshea mifugo kijijini hapo.