Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Zaidi ya Bilioni 8 za TASAF zakuza Uchumi Iringa


Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Halima Dendego akiongea na Timu ya Wadau wa Maendeleo walipofika ofisini kwake ili kujitambulisha

Zaidi ya bilioni 8 zimeingizwa kwenye mzunguko na kukuza uchumi katika Mkoa wa Iringa kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa unaotekelezwa Mkoani humo.  Fedha hii imeingizwa Mkoani humo kupitia Uhawilishaji wa Fedha, Ajira za Muda, Shughuli za Kukuza Uchumi wa Kaya kupitia vikundi mbalimbali vya Kuweka Akiba na Kukopeshana na Ruzuku ya Uzalishaji.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Halima Dendego tarehe 31.01.2024 wakati akiongea na Timu ya Wadau wa Maendeleo walipofika ofisini kwake ili kujitambulisha wakati wakiwa kwenye ziara ya kukagua maendeleo ya Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa 

“Fedha zilizotolewa zimeleta mabadiliko makubwa kwa walengwa kwani kwenye kaya zao sasa wanaweza kupata milo mitatu ya chakula, watoto wadogo ambao walikuwa hawahudhurii klinili sasa Wanahudhuria, waliokuwa hawaendi shule sasa wanakwenda, wameboresha makazi na kujenga nyumba bora, wamekuwa nadhifu katika mavazi, lakini pia wamepata ujuzi na maarifa mbalimbali kupitia miradi wanayoitekeleza”, alisema Mhe. Dendego.

Mkuu wa Mkoa huyo alisema kuwa fedha wanazopewa Wanufaika wa TASAF zinaingia kwenye mzunguko wa maisha ya kawaida na kusaidia kukuza uchumi wa mkoa wa Iringa na kuufanya mkoa kuwa na mzunguko mkubwa wa fedha kwa namna moja au nyingine.

Akiongea baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za TASAF kwa Mkoa wa Iringa, Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Bw. Stanley Magesa aliupongeza uongozi wa Mkoa wa Iringa kwa usimamizi mzuri wa Mpango kwa kuwa wanatekeleza vizuri miradi yote ya TASAF kama ilivyopangwa.

Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Bw. Stanley Magesa akiongea na Wanahabari katika Kijiji cha Iramba, Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa

“Taarifa inaonesha wazi kwamba Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa Mkoani Iringa unatekelezwa vizuri kiasi cha kutupa matumaini kwamba huko vijijini tunakokwenda tutathibisha haya yaliyomo kwenye taarifa hizi”, alisema Bw. Magesa.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa Mkoani Iringa, Mratibu wa TASAF Mkoa wa Iringa, Bi. Saida Mgeni amesema kuwa jumla ya kaya 30,796 zinanufaika na TASAF, jumla ya Miradi 412 ya Ajira Muda imetekelezwa katika vijiji na mitaa 412 na jumla ya Walengwa 15,278 walishiriki kuitekeleza miradi hiyo Mkoani humo.