Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Walengwa TASAF wajenga madaraja, barabara ya mtaa


Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete (katikati) akikagua ujenzi wa moja ya madaraja yaliyojengwa na walengwa wa TASAF eneo la Kinegemgosi manispaa ya Iringa. Kushoto kwake ni Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Rita Kabati na Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TASAF Oscar Maduhu

Walengwa wa TASAF katika Kata ya Ruaha Manispaa ya Iringa wamejenga madaraja mawili ambayo yamesaidia kuondoa adha ya ukosefu wa mawasiliano katika eneo la Kinegemgosi hasa katika misimu ya mvua.

Madaraja hayo yenye  thamani ya shilingi milioni 4.6 yametengenezwa sambamba na ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita moja, ikiwa ni  utekelezaji wa  miradi ya ajira za muda unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF. Ujenzi wa miradi hiyo ulifanyika baada ya kuibuliwa na wananchi wenyewe kutokana na uhitaji uliopo kwenye maeneo yao.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Iringa  Veronica Kessy na Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Jesca Msambatavangu  waliipongeza TASAF kwa utekelezaji wa afua mbalimbali za kuondoa umaskini kwa  kaya za walengwa na kuongeza kuwa mpango wa kunusuru kaya masikini umesaidia kuboresha hali za maisha ya wananchi.

“Sasa hivi walengwa wengi wamefanikiwa kuboresha makazi yao, pia wanafanya biashara mbalimbali ambazo zinawasaidia kuongeza kipato cha kaya zao hivo kujiletea maendeleo,” alisema Mkuu wa Wilaya, kauli iliyoungwa mkono na mbunge wa jimbo la Iringa mjini.

Katika kipindi cha kutoka Julai 2022 na Juni 2023, Halmashauri ya Iringa ilipokea jumla ya shilingi bilioni 1.563 ambapo kati ya hizo shilingi bilioni 1.27 zilikuwa kwa ajili ya ruzuku ya walengwa na shilingi milioni 36.4 za usimamizi, ufuatiliaji wa miradi pamoja na manunuzi ya vifaa.