Habari
TASAF yashiriki Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Dodoma

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF unashiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ambayo yameanza rasmi August 1,2025 katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Maonesho hayo yamebebwa na Kauli Mbiu ya "CHAGUA VIONGOZI BORA KWA MAENDELEO ENDELEVU YA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI 2025"
Katika Maonesho hayo ambayo yamefunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, yanatoa fursa kwa kutembelea maonesho hayo na kujifunza mambo mbalimbali yahusuyo kilimo; ambapo wageni mbalimbali wameendelea kumiminika katika Banda la TASAF ili kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa.
Miongoni mwa wa wageni waliopita katika Banda la Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ni Mkurugenzi Mtendaji (DED) wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bi Asia Juma Messos ambaye amefurahishwa kwa namna ambavyo TASAF imekuwa ikifanya kazi hususani kuwainua Walengwa Tanzania Bara na Visiwani.
DED Asia pia amepata nafasi ya kuwaona walengwa ambao wametoka Unguja, Dar es Salaam pamoja na Dodoma, Bahi, na Kondoa wakiendelea na shughuli ya kuonesha bidhaa walizo nazo na kuwauzia wateja mbalimbali waliofika katika Banda hilo.
Aidha ametoa Wito kwa Walengwa kutumia vizuri fursa waliyoipata ili kuweza kutimiza ndoto zao, huku akiitaka TASAF kuendelea kutoa elimu ili wale wote wanaostahili kutoka katika Mpango watoke bila malalamiko kati yao na Serikali lakini pia kuruhusu wengine waweze kuingia katika Mpango muda utakapofika.
Nao baadhi ya Walengwa wameipongeza TASAF na Serikali kwa elimu waliyopata kwani kabla ya kuingia TASAF hali zao kimaisha zilikuwa duni, lakini kwa sasa wanaweza kujimudu kimaisha.
Mbali na DED wa Mkalama pia Mkurugenzi wa Mifumo, Tathmini na Mawasiliano TASAF Bwana Japhet Boaz pamoja na Meneja wa Masijala ya Walengwa nao ni miongoni mwa wageni waliofika katika Banda la TASAF.
Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo, maarufu kama Nanenane yanategemewa kufungwa siku ya Ijumaa ya tarehe 8/08/2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Viwanja vya Maonesho Nzuguni.