Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Simbachawene afafanua utaratibu Ajira za Muda


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amefafanua utaratibu wa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa kushiriki kazi za ajira za muda.

Akiwa katika ziara ya kukagua shughuli za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF wilayani Mkinga mkoani Tanga Jumanne Oktoba 17, 2023 Waziri Simbachawene amesema ni muhimu kwa wanufaika na watekelezaji wa mradi mdogo wa Ajira za Muda kuzingatia masharti ya kushiriki katika shughuli hizo.

Ameyataja masharti hayo kuwa ni mshiriki kuwa na umri kati ya miaka 18 na 65, kuwa na kuwa na afya njema. Simbachawene alisisitiza hayo baada ya kutembelea barabara iliyojengwa kwa nguvu za walengwa katika mradi wa Ajira za Muda na kupata maelezo ya utekelezaji wa mradi huo.

Akifafanua kuhusu lengo la miradi ya ajira za muda na kwa nini walengwa ndio wanafanya kazi hizo Mhe. Simbachawene alisema

“Sio lengo la Serikali kuwafanya mlime barabara kwa mikono, bali ni kutoa ajira kwenu baada ya kufanya kazi ikiwa pia ni njia ya kuwafundisha kujitegemea,”

Akizungumza malalamiko kuwa watu wasio na sifa wanaingizwa kwenye Mpango wakati wenye sifa wanaachwa, amesema kuwa kama hilo lipo basi ni makosa ya wana jamii wenyewe na watendaji vijijini kwa kuwa walengwa huchaguliwa na wananchi wenyewe katika Mkutano Mkuu wa Kijiji.

Amewataka wananchi kuwa makini kila inapotokea fursa ya utambuzi wa Kaya za kuingia kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini. Alimaliza kwa kuwaeleza wananchi kuwa kwa sasa hakutafanyika utambuzi wa walengwa wapya hadi Kipindi hiki cha pili cha Mpango kitakapokamilika.