Habari
Waziri Simbachawene aambatana na uongozi wa TASAF katika ziara nchini Afrika Kusini

Waziri ya Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora Mhe. George Boniface Simbachawene pamoja na viongozi waandamizi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF wanafanya ziara ya mafunzo nchini Afrika Kusini kwa lengo la kujifunza kuhusu namna bora ya utekelezaji wa mradi wa ajira za muda inayotekelezwa na TASAF.
Mafunzo hayo ya siku tano yameanza Machi 17, 2025 hadi Machi 23, nchini Afrika Kusini na ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Mhe. Simbachawene, pamoja na viongozi waandamizi wa TASAF akiwemo Mkurugenzi Mtendaji, Shadrack Mziray.
Ziara hiyo imeratibiwa na Mfuko wa Nchi zinazotoa Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC FUND) ikijumuisha wadau mbalimbali wanaohusika moja kwa moja na utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ikiwemo Ofisi ya Rais -Ikulu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Wizara ya Fedha.
Mafunzo hayo yanawawezesha Serikali pamoja na watendaji kupata weledi zaidi katika utekelezaji wa ajira za muda za TASAF katika awamu nyingine.
Awali kabla ya kuanza ziara hiyo, Mhe. Simbachawene na ujumbe wake walitembelea ofisi za ubalozi Tanzania nchini mjini Pretoria kwa lengo la kusaini kitabu cha wageni pamoja na kusalimia watumishi.
Pia alifanya mazungumzo na balozi wa Tanzania nchini Afrika ya Kusini Mhe James Bwana, kuhusiana na maboresho yaliyofanyika na kujenga mifumo inayowezesha kutataua changamoto za kiutumishi kwa urahisi kwa watumishi wote wakiwemo walio katika balozi mbalimbali duniani.
Mhe. Simbachawene alimweleza Balozi kuwa TASAF imewezesha kuwakwamua wananchi kiuchumi sambamba na kuboresha miundombinu katika maeneo mbalimbali ya vijijini ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, shule, nyumba za walimu ili kurahisisha huduma za elimu kwa wanafunzi wa maeneo hayo.
“TASAF imekuwa suluhu ya kuwaondoa wananchi kwenye umasikini, hivyo,tunapokuja katika mafunzo kama haya inatusaidia katika kujiandaa na awamu nyingine za mradi wa kupambana umasikini,” alisema.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Afrika ya Kusini Mhe. James Bwana alimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri inayofanywa na Wizara yake na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya kila siku.
Wakiwa katika ziara hiyo walitembelea miradi ya barabara ikiwemo ukarabati unaotekelezwa na Idara ya Barabara na Usafirishaji ya Gauteng.
Mradi huu unahusisha ukarabati wa barabara ya P122, inayounganisha mji wa Olifantsfontein hadi Solomon Mahlangu Drive, na barabara ya K101 kutoka D795 Midrand hadi N1 Brakfontein yenye urefu wa takriban kilomita 54.