Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Waziri Simbachawene aeleza Mafanikio ya TASAF katika Miaka 60 ya Muungano


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameueleza umma kuwa katika kipindi cha Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF imefanikiwa kupunguza kiwango cha umaskini uliokithiri kwa Walengwa kwa asilimia 8 kwa kuongeza uwezo wa kaya kumudu gharama za mahitaji ya msingi ya kaya kwa asilimia 10.

Waziri Simbachawene ameongeza kuwa katika miaka 60 ya Muungano kumekuwa na kuongezeka kwa idadi ya walengwa wanaoshiriki katika shughuli za kilimo na ongezeko la matumizi ya pembejeo ambazo zimeongeza tija kwenye uzalishaji wa mali za kaya na kuchangia kukuza uchumi wa nchi.

Hayo ameyazungumza Mhe. Simbachawene tarehe 15 Aprili 2024 alipofanya Mkutano na Wanahabari wakati akieleza mafanikio ya miaka 60 ya Muungano kwa Taasisi za Kimuungano zilizopo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ikiwemo TASAF, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa PSSSF jijini Dodoma

“Mafanikio mengine ya TASAF ni ongezeko la uandikishwaji na mahudhurio shuleni kwa watoto kutoka kaya maskini kwa asilimia 6; ongezeko la matumizi ya huduma za afya miongoni mwa kaya za walengwa na kuongezeka kwa mahudhurio kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa watoto wenye umri kati ya miezi 0 - 24 kutoka kaya maskini; kuongezeka kwa akiba na rasilimali za kaya ambazo zinawezesha kaya kujikinga na majanga yanapotokea na kuboresha makazi ya Kaya kwa kujenga nyumba bora kwa kutumia matofali ya kuchoma au saruji na kupaua kwa mbao na kuzifunika kwa bati”, alisisitiza Waziri Simbachawene.

Aidha, Waziri Simbachawene amesema kuwa hadi kufikia Machi, 2024, walengwa wamepewa mafunzo ya stadi za msingi za kuendesha shughuli za kiuchumi kwa pande zote za Muungano ikiwa kwa Tanzania Bara jumla ya walengwa 27,964 kutoka Halmashauri 33 walipatiwa mafunzo na Ruzuku ya Uzalishaji ya kiasi cha shilingi bilioni 8.6 na Unguja na Pemba walengwa 23,399 walipatiwa mafunzo na walipewa ruzuku ya kiasi cha shilingi bilioni 8.9 ikiwa ni fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi yao ya kuzalisha na kuongeza kipato cha Kaya.

Akiendelea kufafanua mafanikio hayo, Mhe. Simbachawene aliongeza kuwa kupitia TASAF, Serikali ya Awamu ya Sita imekuza uchumi wa Kaya Maskini kwa kuhamasisha Walengwa kuunda vikundi vya kuweka akiba, kukopeshana na kuwekeza kwenye miradi ya uzalishaji mali ili kuinua kipato cha Kaya.

“Kwa Tanzania Bara jumla ya vikundi vya kuweka akiba 26,842 vyenye wanachama 358,846 viliundwa katika Mamlaka za Maeneo ya Utekelezaji na kuweza kuweka akiba ya kiasi cha Shilingi bilioni 6.3; na kwa upande wa Unguja na Pemba, jumla ya vikundi 3,211 vyenye wanachama 45,948 vimeundwa na vimeweza kukusanya jumla ya akiba ya shilingi bilioni 1.6 na kuweza kukopeshana kwa wanachama”, alifafanua Mhe. Simbachawene.

Taasisi za Kimuungano zilizopo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, mbali na TASAF ni Sekretarieti ya Ajira ambayo pia Mhe. Waziri alipata muda wa kueleza mafanikio yake Kimuungano.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (wa pili kushoto) na Maofisa wengine wakimsikiliza Naibu Mkurugenzi wa Habari Maelezo Bi. Zamaradi Kawawa kabla ya kumkaribisha Waziri

Naibu Mkurugenzi wa Habari Maelezo Bi. Zamaradi Kawawa akitoa neno la Utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kuzungumza na vyombo vya habari juu ya Mafanikio ya Miaka 60 ya Muungano

Baadhi ya Wanahabari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumzia Mafanikio ya Miaka 60 ya Muungano