Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Waziri Simbachawene ziarani Geita kukagua shughuli za TASAF


Waziri wa Nchi Ofisi ya ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora George Simbachawene ameuagiza uongozi wa TASAF kubuni njia bora zaidi ya kuwalipa wazee na wasiojiweza ili kuondoa changamoto ya wizi unaofanywa na ndugu au watu wanaowasaidia kutoa fedha za mpango kwa njia za simu.

Waziri Simbachawene ametoa agizo hilo leo Septemba 13,2023 mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa mpango wa TASAF mkoani Geita ambapo amesisitiza umuhimu wa kutoa malipo kwa simu na kwamba umelenga kupunguza gharama za uendeshaji lakini sasa hatua mpya zinapaswa kuchukuliwa kutokana na changamoto ya fedha hizo kutowafikia baadhi ya walengwa kwa kukosa uwezo wa kutumia simu.

“Tuangalie upya namna tunavyowalipa hawa wazee ili tuwaondolee hii changamoto ya kuibiwa najua mna mifumo yenu wakati mkitaka kuiboresha basi angalieni njia bora itakayo wawezesha wapate fedha hizi”. Amesema Waziri Simbachawene.

Kuhusu fedha zinazotolewa kwa walengwa wasio na sifa, Waziri Simbachawene ameagiza kusitishwa kwa fedha hizo mara moja na badala yake zipangiwe kazi nyingine wakati mpango wa kuwapata mpango wa kuwapata walengwa wenye sifa ukiendelea.

Akizungumzia fedha zinazotolewa na TASAF kwa ajili ya miradi mbalimbali katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Simbachawene Mkoa wa Geita umepokea zaidi ya Sh100 bilioni ambazo zimetumika kwenye ujenzi wa miundombinu katika sekta za elimu, afya, kulipa wazee na wasiojiweza pamoja na ujira kwa ajili ya wafanyakazi wa ajira za muda.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Geita, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Mipango na Uratibu Deodatus Kayango amesema Mpango wa TASAF unazihudumia kaya 46,749 zenye walengwa 220,666 ambapo kwa kipindi cha pili cha awamu ya tatu zaidi ya Sh 35.4 milioni zimelipwa kwa walengwa.

Amesema katika kipindi cha mwaka 2021-2023 Mkoa wa Geita ulipokea Sh 8.09 bilioni kwa ajili ya miradi ya kuondoa umaskini ambayo ni ujenzi wa miundombinu ya Elimu, Afya, miradi ya ajira za muda pamoja na miradi ya vikundi kwa walengwa.

Katibu Tawala Msaidizi huyo pia ameyaainisha mafanikio yaliyopatikana kupitia mpango huo wa TASAF, ikiwemo kaya za walengwa kupata mahitaji kwa ajili ya Watoto ambao ni wanafunzi kupata elimu ya msingi na sekondari lakini pia kuwawezesha watoto chini ya mikaa mitano kupata matibabu.

“Mafanikio mengine ni walengwa kumudu kupata mahitaji ya msingi ikiwemo ikiwemo kumudu kupata milo miwili kwa siku kutoka kwenye mlo mmoja waliokuwa wakipata awali pamoja na kufanikiwa kuezeka nyumba kwa bati kutoka nyumba za nyasi zilizokuwepo.” Amesema Bw. Kayango

Waziri Simbachawene ameanza ziara ya siku tatu mkoani Geita ambapo, katika siku ya kwanza baada ya kulakiwa na Mkuu wa Mkoa Martin Shigella ametembelea mradi wa ujenzi wa jengo la utawala katika shule ya Sekondari Inyala Wilayani Geita unaotekelezwa na TASAF.