Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Naibu Waziri Aipongeza TASAF kwa Kubadilisha Maisha ya Kaya Maskini


Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege Qwaray, ameupongeza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) kwa mchango wake mkubwa katika kuwawezesha wananchi walio katika mazingira magumu na kaya maskini kukabiliana na changamoto za kiuchumi, kuboresha maisha yao na kujitegemea.

Mhe. Qwaray alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la TASAF katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

Alisema TASAF imeendelea kutekeleza kampeni mbalimbali za uhamasishaji wa umma kuhusu fursa zinazopatikana kupitia programu zake, jambo ambalo limeziwezesha kaya maskini kuelewa kwa urahisi zaidi na kunufaika na huduma zinazochangia maendeleo yao ya kijamii na kiuchumi.

“Ninaipongeza TASAF kwa kazi nzuri mnayoifanya. Endeleeni kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kuinua uchumi wa wananchi na kujenga Tanzania yenye ustawi kwa kuwawezesha watu kujitegemea badala ya kutegemea misaada,” alisema.

Naibu Waziri huyo alibainisha kuwa afua za TASAF zimekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha ustawi wa makundi mbalimbali yaliyo katika mazingira magumu nchini kwa kuyawezesha kushiriki katika shughuli za uzalishaji na kuboresha hali zao za kiuchumi.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, aliipongeza TASAF kwa kuendelea kutoa msaada wa elimu kwa watoto wanaotoka katika kaya maskini, akisema programu hiyo imewawezesha walengwa wengi kuendelea na masomo yao licha ya changamoto za kifedha zinazozikabili familia zao.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego, akiangalia  bidhaa zinazotengenezwa na wanufaika wa TASAF wakati wa maeonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika jijni Dodoma

Alisema uwekezaji wa TASAF katika sekta ya elimu unasaidia kujenga mustakabali bora kwa watoto wanaotoka katika mazingira yasiyojiweza na kuchangia kupunguza umaskini kwa muda mrefu.

“Kusaidia elimu ya watoto ni moja ya njia bora zaidi za kuvunja mzunguko wa umaskini. Mchango wa TASAF katika eneo hili umesaidia familia nyingi kuhakikisha watoto wao wanapata mustakabali mzuri zaidi,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Mhe. Gift Msuya, alisema viongozi wa wilaya hukutana mara kwa mara na watoto wenye uwezo mkubwa kitaaluma ambao wanashindwa kufikia ndoto zao za elimu kutokana na changamoto za kifedha.

Mkuu wa Wilaya ya Pangani Mhe. Gift Msuya akizungumza na wanufaika wa TASAF wakati wa maeonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika jijni Dodoma

Kutokana na hali hiyo, aliiomba TASAF kuangalia uwezekano wa kuweka utaratibu utakaowezesha mamlaka za serikali za mitaa kutambua na kusaidia kaya zenye uhitaji, ikiwemo zile zilizopo maeneo ya mijini ambazo wakati mwingine haziwezi kufikiwa kupitia mchakato wa kawaida wa usajili wa programu za TASAF.

“Tuna kaya nyingi katika maeneo ya mijini zinazokabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi ambazo bado hazijafikiwa na programu za TASAF. Ni muhimu kuangalia namna ya kuzitambua na kuzifikia ili nazo ziweze kunufaika na huduma hizi,” alisema Mhe. Msuya.

Aidha, aliiomba TASAF kutoa kipaumbele maalum kwa kaya zinazolea watoto yatima waliopoteza wazazi wao, akibainisha kuwa familia hizo mara nyingi huhitaji msaada wa ziada ili kuwawezesha watoto hao kuendelea na masomo yao pamoja na maisha ya kila siku bila vikwazo vikubwa vya kiuchumi.