Habari
Kikwete atembelea banda la TASAF, awapongeza walengwa
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, ametembelea banda la Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Akiwa katika banda hilo, Waziri Kikwete amesalimiana na walengwa wa TASAF na kusaini kitabu cha wageni, huku akipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazofanywa na wanufaika wa mfuko huo.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, naye ametembelea banda hilo jana na kuwapongeza walengwa kwa juhudi wanazofanya kujikwamua kiuchumi kupitia miradi mbalimbali ya uzalishaji mali.
Mbali na kuwapongeza, Mkomi alinunua baadhi ya bidhaa zilizozalishwa na walengwa hao, akisema hatua hiyo ni sehemu ya kuwaunga mkono ili waendelee kuimarisha shughuli zao za kiuchumi na kuongeza kipato cha familia zao.
Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanaendelea katika Viwanja vya Chinangali, Dodoma, yakihusisha taasisi mbalimbali za umma zinazotoa huduma kwa wananchi.
