Habari
TASAF na HESLB zashirikiana kutoa elimu kwa waombaji wa mikopo mwaka 2026/2027
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) tunatoa elimu na huduma ya upatikanaji wa viambatanisho kwa waombaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
Shughuli hiyo inafanyika katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mbeya, Dar es Salaam, Kagera, Kilimanjaro, Tabora, Mtwara, Dodoma, Arusha na Zanzibar (Unguja na Pemba).

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Meneja wa HESLB Kanda ya Ziwa, Bw. Usama Choka, amesema taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha waombaji wote wanapata taarifa sahihi na kwa wakati ili kuongeza uelewa na kupunguza changamoto zinazojitokeza wakati wa uombaji wa mikopo.
“Tunawakaribisha wanafunzi, wazazi na wadau wote kujitokeza katika vituo hivi ili kupata elimu sahihi kuhusu uombaji wa mikopo ya elimu ya juu na vyuo vya kati, kwani lengo letu ni kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekosa taarifa muhimu”, amesema Choka.
Kwa upande mwingine, TASAF imesema ushiriki wake katika zoezi hilo unatokana na mkataba wa maelewano uliopo kati yake na HESLB unaolenga kusaidia watoto kutoka kaya maskini kupata fursa ya elimu ya juu kwa kuwapatia mikopo kwa asilimia 100.
“Ushirikiano huu ni sehemu ya dhamira yetu ya kuhakikisha watoto wa kaya maskini wanaendelea kupata fursa ya elimu ya juu bila vikwazo vya kifedha, kupitia mfumo uliowekwa kwa ushirikiano na HESLB kwa kuwa kupata elimu ya chuo kikuu ni moja ya njia za kuondokana na umaskini”, imeeleza TASAF.
Baadhi ya wanafunzi waliofika katika kituo cha Rock City jijini Mwanza wameeleza kufurahishwa na huduma hiyo wakisema imewasaidia kupata uelewa wa moja kwa moja kuhusu hatua za maombi ya mikopo na vigezo vinavyotumika.

“Huduma hii imetusaidia kupata majibu ya maswali yetu kwa wakati na kutuondolea hofu kuhusu namna ya kuomba mikopo kwa usahihi na kwa wakati. Tunawasihi wanafunzi wenzetu wote wanaotegemea kuomba mikopo bodi ya mikopo wafike kupata elimu ili kupunguza changamoto wakati wa kuomba ukifika”, amesema mmoja wa wanafunzi waliohudhuria kituoni hapo.
Ushirikiano wa TASAF na HESLB ni hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa elimu ya juu kwa watoto wa kaya maskini, huku taasisi hizo zikisisitiza kuwa elimu sahihi kwa waombaji ni msingi wa kuhakikisha wanufaika wanafikia huduma hiyo kwa usahihi, kwa wakati na kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa.
