Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

TASAF yaendelea kubadili maisha ya wananchi Zanzibar


Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema kuwa Serikali imeendelea kusimamia kwa mafanikio utekelezaji wa Programu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Mhe. Abdulla ameyasema hayo wakati akiwasilisha katika Baraza la Wawakilishi hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Amesema katika kipindi cha utekelezaji wa awamu ya tatu ambayo ilikamilika mwezi Septemba 2025, Serikali iliratibu na kusimamia zoezi la majaribio la uibuaji wa walengwa wa kaya masikini lililofanyika katika Shehia 75 za Unguja na Pemba, likihusisha jumla ya kaya 13,919, ambapo kaya 899 ni za Unguja na 13,020 za Pemba.

“Zoezi hilo lililenga kukusanya taarifa muhimu kuhusu viashiria vya umasikini vinavyotokana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Mhe. Abdulla.

Aidha, ameeleza kuwa TASAF ilitoa ruzuku ya uzalishaji yenye thamani ya shilingi 41,994,281 kwa kaya 135 za walengwa wa Unguja, hatua iliyolenga kuwawezesha kiuchumi wananchi hao.

“Kadhalika, Serikali imeratibu na kusimamia malipo kwa kaya masikini ambapo jumla ya shilingi 1,750,993,473 zimetolewa kwa kaya 27,886 katika Unguja na Pemba, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza umasikini,” aliongeza.

Kwa upande wa sekta ya elimu, amesema kuwa jumla ya shilingi 347,526,500 zilitumika katika ujenzi wa madarasa 19 katika skuli tatu ambazo ni Kendwa (madarasa 7), Mtangani (madarasa 5) na Dodo (madarasa 7), hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

Aidha, Mhe. Abdulla amesema kuwa katika bajeti ya mwaka 2025/2026, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepanga kutoa mchango wa shilingi 100,000,000 kwa ajili ya kuendeleza shughuli za TASAF.

Amesisitiza kuwa juhudi hizo zinaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha ustawi wa jamii na kupunguza umasikini kwa wananchi wa Zanzibar