Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

TASAF yaimarisha Kinga ya Jamii kupitia Teknolojia


Wakati Tanzania ikiimarisha ajenda ya mageuzi ya kidijitali, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) unaendelea kuwa mfano thabiti wa namna teknolojia inavyoweza kuboresha utoaji wa huduma na kuimarisha uwajibikaji wa pamoja katika programu za kinga ya jamii.

Kupitia uwekezaji wa kimkakati katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), TASAF imeongeza kwa kiwango kikubwa ufanisi, uwazi na wigo wa utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (PSSN), na hivyo kunufaisha mamilioni ya kaya zilizo katika mazingira magumu nchini kote.

Katika kuelekea utekelezaji wa awamu ya tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (PSSN III), TASAF inaendeleza dhamira yake ya kufanya teknolojia kuwa msingi wa utoaji wa huduma bora na kwa wakati.

Akizungumza kuhusu safari ya taasisi katika mageuzi ya kidijitali, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Shedrack Mziray, alisema kuwa ujumuishaji wa TEHAMA umekuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha mifumo ya kinga ya jamii inafanya kazi kwa uadilifu na usahihi.

“Teknolojia imeimarisha kwa kiasi kikubwa namna TASAF inavyotoa huduma,” alisema Mkurugenzi Mtendaji. “Kupitia mifumo ya kidijitali, tunaweza kuhakikisha kuwa malipo yanawafikia walengwa sahihi, malipo yanachakatwa kwa ufanisi, na utendaji unafuatiliwa kwa wakati halisi. TEHAMA si chaguo tena; bali ni msingi wa utoaji bora wa huduma.”

TASAF imehama kutoka mifumo ya kiutawala ya karatasi kwenda kwenye majukwaa ya kidijitali yaliyoundwa na serikali kusimamia shughuli kubwa za kitaifa. TASAF imetengeneza Mfumo wa taarifa za usimamizi wa TASAF-MIS, jukwaa jumuishi la kidijitali linalosaidia uandikishaji wa walengwa, upangaji wa vigezo vya ustahiki, uchakataji na uhawilishaji wa malipo ya walengwa, ufuatiliaji wa masharti, na utoaji wa taarifa.

Mfumo wa TASAF MIS unaruhusu taarifa zinazokusanywa katika ngazi ya jamii kusafirishwa kwa usalama na kupatikana katika ngazi za Halmashauri, Mkoa na Taifa. Muunganiko huu unapunguza urudufu wa taarifa, unaimarisha usahihi wa takwimu na kuongeza usimamizi, uwazi na uwajibikaji. Viongozi wanaweza kuzalisha taarifa kwa haraka, kuchambua mwenendo wa utekelezaji wa Mpango na kubaini mapungufu bila kusubiri ukusanyaji wa taarifa kwa njia ya mkono.

Wanafunzi wa shule ya Sekondari Igogwe Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, wakifurahia miundombinu ya kujifunzia kwa vitendo masomo ya Sayansi. Shule hiyo imejengwa na TASAF kupitia awamu ya nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania.

Uwekaji wa mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa walengwa umeimarisha kwa kiasi kikubwa uadilifu wa programu.

“Mifumo yetu ya kidijitali imeongeza uwazi na kupunguza makosa,” alibainisha Mkurugenzi Mtendaji. “Sasa tuna takwimu zilizopangwa vizuri zinazosaidia katika kufanya maamuzi. Hii inaongeza uwajibikaji ndani ya taasisi na pia kwa wananchi tunaowahudumia.”

Hatua nyingine ya mageuzi makubwa imekuwa ni matumizi ya mfumo wa malipo kwa njia za kielektroniki (e-payment). Badala ya kutumia gharama kubwa kufikisha fedha taslimu kwa walengwa waliopo nchi nzima, TASAF inashirikiana na watoa huduma za fedha ikiwa ni pamoja na makampuni ya simu na benki, kupeleka fedha moja kwa moja kwenye akaunti za benki au simu za walengwa na kuwafikia kwa haraka na popote walipo. Miundombinu hii ya kielektroniki inahakikisha kila muamala unasajiliwa, unathibitishwa na unaweza kufuatiliwa ndani ya mfumo.

Jumla ya kaya za walengwa 535,536 nchini kote, walipokea ruzuku zao kupitia akaunti za benki na mitandao ya simu wakati wa utekelezaji wa Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Fedha huingizwa moja kwa moja kwenye akaunti zao za benki au mitandao ya simu na walengwa wanaweza kuzitoa kwa mawakala waliopo karibu na makazi yao. Mfumo huu umepunguza hatari zilizokuwa zikihusiana na upokeaji wa fedha taslimu kama vile kuibiwa, kupoteza na hata kufanya matumizi yasiyo sahihi.

Walengwa wameonesha imani kubwa katika mfumo wa malipo ya kielektroniki. Wanathibitisha kuwa fedha zinafika kwa wakati uliopangwa. Mfumo huu pia umepunguza misongamano ya walengwa siku ya malipo ambapo walitumia muda mwingi kusubiri fedha zao. Sasa walengwa wanapata muda mwingi wa kufanya shughuli za kuongeza kipato cha kaya kwani wanapata fedha zao popote walipo.

Malipo ya kielektroniki pia yamepanua ujumuishaji wa kifedha kwa walengwa wa TASAF. Walengwa wengi, hususan wanawake wa vijijini, wamefungua akaunti za benki na za mitandao ya simu ambazo zinawafanya wafurahie bidhaa mbali mbali zinazotolewa na watoa huduma hao za kifedha kama mikopo, akiba na mafunzo.

Hii imewawezesha si tu kupokea ruzuku, bali pia kuweka akiba, kufanya miamala mingine na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi. Hivyo, matumizi ya TEHAMA katika malipo yameimarisha uwezeshaji wa kiuchumi na hadhi ya kijamii. Bw. Mziray alisisitiza matokeo chanya ya kijamii za mfumo huu.

“Malipo ya kielektroniki yanaongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za TASAF, Walengwa wanapokea fedha zao kwa usalama na uwazi. Hii inajenga imani katika mfumo na kupunguza mianya ya udanganyifu.”

Mbali na utoaji wa huduma moja kwa moja, kanzidata imara ya walengwa ya TASAF imekuwa rasilimali muhimu ya kitaifa. Takwimu zilizokusanywa na kuthibitishwa sasa zinasaidia mipango mipana ya serikali na uratibu wa huduma za kijamii.

Hususan, kanzidata hiyo inatumika katika programu mbalimbali za kitaifa, ikiwemo mpango wa Bima ya Afya kwa Wote uliozinduliwa hivi karibuni, ambapo husaidia utambuzi sahihi wa kaya zinazostahili. Aidha, kanzidata ya TASAF inasomana na mifumo ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ambapo husaidia kuwatambua wanafunzi waliotoka Kaya za Walengwa wa TASAF waliodahiliwa kwenye vyuo vya elimu ya juu na kati, kisha kuwapatia mikopo kwa asilimia 100.

Kupitia mifumo ya kuunganisha taarifa na ushirikishanaji salama wa data, rejista ya walengwa ya TASAF inasaidia kubaini makundi yaliyo katika mazingira magumu yanayostahili kupata huduma za afya kwa gharama nafuu au kwa ruzuku.

Muunganiko huu unapunguza urudufu kati ya programu na kuhakikisha msaada wa serikali unalengwa kwa usahihi na kuendeshwa kwa misingi ya takwimu. Matumizi ya kanzidata moja iliyothibitishwa yanaimarisha uratibu wa sera na kuimarisha mfumo wa kinga ya jamii nchini.

Uwezo wa kuunganisha takwimu za kinga ya jamii na mifumo mingine ya kitaifa unaonyesha umuhimu wa kimkakati wa uwekezaji katika TEHAMA. Kwa kuzalisha takwimu za kuaminika katika ngazi ya kaya.

Zaidi ya malipo, TEHAMA imeongeza uwezo wa TASAF katika ufuatiliaji na tathmini. Dashibodi za kidijitali zinatoa taarifa kwa wakati halisi kuhusu utendaji wa mikoa, wigo wa walengwa na viwango vya uzingatiaji wa masharti. Uwazi huu unaimarisha usimamizi na kuwezesha hatua za marekebisho kuchukuliwa kwa wakati.

Mnufaika wa TASAF akisaini malipo ya ruzuku yanayotolewa kwa njia za kielekroniki (kidijitali) ikiwa ni sehemu ya matumizi ya teknolojia katika utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Katika mazingira ambayo ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma unaongezeka, uwazi huu ni muhimu. Teknolojia inaiwezesha TASAF kuonesha matokeo yanayopimika na kuimarisha imani ya umma katika matumizi sahihi ya rasilimali za taifa.

Mfumo wa kushughulikia malalamiko nao umeimarishwa kwa kuingizwa katika mfumo wa kidijitali. Wananchi wanaweza kuwasilisha malalamiko yanayohusu ustahiki, upangaji au malipo, na malalamiko hayo hufuatiliwa kimfumo hadi kupatiwa ufumbuzi. Mfumo huu unapunguza muda wa majibu na kuongeza uwajibikaji katika ngazi zote.

“Dhamira yetu ni kuhakikisha hakuna malalamiko yanayopuuzwa,” alisema. “Kupitia ufuatiliaji wa kidijitali wa malalamiko, tunaweza kufuatilia muda wa majibu na kubaini changamoto zinazojirudia. Hii inaongeza haki na uwajibikaji.”

Hata hivyo, matumizi ya teknolojia yamekwenda sambamba na kuimarisha taasisi. TASAF imewekeza katika mafunzo kwa watumishi, ulinzi wa mifumo dhidi ya udukuzi, na mifumo sanifu ya utoaji wa taarifa ili kuhakikisha uendelevu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mifumo, Tathmini na Mawasiliano Bw. Japheth Boaz, alisisitiza kuwa mageuzi ya kidijitali yanahusu watu na mifumo sawa na programu za kompyuta.

“Teknolojia lazima iungwe mkono na watumishi wenye ujuzi na mifumo imara ya utawala,” alisema. “Tunajenga uwezo wa ndani kuhakikisha mifumo yetu ya kidijitali inabaki salama, ya kuaminika na yenye kuitikia mahitaji.”

TASAF inapojiandaa kwa utekelezaji wa Mpango unaofuata wa Imarisha Kaya (PSSN III), jukumu la TEHAMA litaongezeka zaidi. Awamu hii inalenga kupanua wigo wa kinga ya jamii, kuimarisha juhudi za kujenga ustahimilivu, na kuongeza uwezo wa programu kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi.

Kupitia uwekezaji endelevu katika TEHAMA, TASAF si tu inaboresha utoaji wa huduma leo, bali pia inaweka msingi wa mfumo wa kisasa wa kinga ya jamii ulio tayari kwa changamoto za baadaye.

Kadiri Tanzania inavyoendelea na safari ya mageuzi ya kidijitali katika taasisi za umma, uzoefu wa TASAF unaonyesha wazi jinsi teknolojia inavyoweza kuimarisha utawala bora, kuongeza uwajibikaji, na hatimaye kuboresha maisha ya mamilioni ya wananchi.