Habari
TASAF yahawilisha bilioni 43.5 kwa Kaya Maskini, Serikali yaweka mikakati mipya
Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imetoa jumla ya shilingi bilioni 43.5 kwa kaya maskini nchini katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza umaskini na kuboresha maisha.
Taarifa hiyo ilisomwa bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Mhe. Kikwete alisema fedha hizo zilihawilishwa kwa kaya 896,746 katika maeneo 186 ya utekelezaji. Aidha, kaya 535,536 sawa na asilimia 60 ya walengwa walipokea ruzuku kupitia mifumo ya kielektroniki ikiwemo mitandao ya simu na akaunti za benki.
Katika kipindi hicho, TASAF pia ilitekeleza miradi 98 ya kijamii iliyowezesha kaya 226,010 kushiriki katika ajira za muda katika sekta za afya, elimu na maji.
Alisema, miradi 78 ya maendeleo ya miundombinu yenye thamani ya shilingi bilioni 2.88 ilipatiwa fedha na ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Maboresho ya TEHAMA na Mpango Mpya
TASAF imeendelea kuboresha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuendana na mahitaji ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Awamu ya Tatu (PSSN III) pamoja na utekelezaji wa Sera ya Kinga ya Jamii.
“Aidha, uchambuzi wa data za tathmini ya mpango huo umekamilika, na matokeo ya awali tayari yamewasilishwa kwa wadau. Mapendekezo yaliyopatikana yametumika kuboresha mpango ujao, hasa katika maeneo ya ruzuku za uzalishaji mali na ajira za muda,” alisema.
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Awamu ya Tatu (PSSN III), unaotarajiwa kugharimu dola za Marekani milioni 300, umeidhinishwa rasmi na Bodi ya Benki ya Dunia Machi 31, 2026, na unatarajiwa kutekelezwa kwa miaka minne kuanzia 2026 hadi 2029.
Mipango ya 2026/27
Alisema, kwa mwaka wa fedha 2026/27, TASAF imepanga kutekeleza shughuli mbalimbali ikiwemo kukamilisha utambuzi na uandikishaji wa kaya zitakazonufaika na mpango huo katika mamlaka 100 Tanzania Bara na Zanzibar.
Pia, ruzuku zinatarajiwa kutolewa kwa kaya 500,000 zitakazokidhi vigezo, huku juhudi zikifanyika kujenga uwezo kwa viongozi na jamii ili kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mpango huo.
“Katika kukabiliana na changamoto za mazingira, miradi ya ajira za muda itatekelezwa katika maeneo 10 yaliyoathirika zaidi na mabadiliko ya kimazingira,” alisema.
Zaidi ya hayo, jumla ya miradi 723 ya maendeleo ya miundombinu ya huduma za jamii inatarajiwa kutekelezwa katika sekta za afya, elimu, maji, mazingira na ujasiriamali katika mamlaka 62 za utekelezaji.
