Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

TASAF yaboresha upatikanaji wa huduma za afya Chamwino


Mfuko wa Maendeleo ya Jamii -TASAF umeendelea kuonesha mchango mkubwa katika kuboresha huduma za afya nchini, ambapo katika Kijiji cha Mgunga, Kata ya Msamalo wilayani Chamwino mkoani Dodoma, wananchi wameeleza kufurahishwa na hatua ya ujenzi wa Kituo cha Afya Msamalo huku wakitoa ombi la kukamilishwa kwa majengo muhimu ya huduma za upasuaji na mama na mtoto ili kuongeza ufanisi wa huduma.

Hali hiyo imebainishwa wakati wa ziara ya wataalamu na wawakilishi kutoka Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania waliotembelea eneo hilo kwa lengo la kukagua maendeleo ya utekelezaji wa awamu ya pili ya mpango wa TASAF pamoja na kujionea namna mradi wa kituo hicho cha afya unavyoendelea kunufaisha jamii ya maeneo ya jirani.

Ujumbe wa wakilishi kutoka Ubalozi wa Uswisi pamoja na watumishi wa TASAF wakipokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino

Katika maelezo yao, wananchi wamesema uwepo wa kituo hicho umekuwa mkombozi mkubwa, lakini bado changamoto ya kukosekana kwa huduma za upasuaji na wodi ya mama na mtoto imeendelea kuwalazimu kusafiri umbali mrefu kufuata huduma katika hospitali za wilaya na rufaa, jambo linaloongeza gharama na wakati wa kupata matibabu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mgunga, Simon Masagasi, amesema ujenzi wa kituo hicho umekuwa hatua muhimu kwa maendeleo ya afya ya jamii, lakini bado kuna hitaji kubwa la kukamilisha miundombinu iliyobaki ili kituo kiweze kutoa huduma zote muhimu kwa wakazi wa eneo hilo na vijiji jirani.

Alieleza kuwa kabla ya uwepo wa kituo hicho, wananchi, hususan wajawazito, walilazimika kutumia usafiri wa mbali na wakati mwingine usio salama kufuata huduma, hali iliyokuwa ikiweka maisha yao hatarini.

Mkazi wa eneo hilo, Mary Sabugo, amesema awali changamoto ya huduma za afya ilikuwa kubwa zaidi, kwani walilazimika kusafiri kwenda maeneo ya mbali hata kwa matatizo madogo ya kiafya, jambo lililokuwa likichelewesha matibabu na kuongeza hatari kwa wagonjwa.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Msamalo,  Dkt. Rebecca Kitundu

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Msamalo, Rebecca Kitundu, amesema kituo hicho kinahudumia zaidi ya wakazi 16,000 kutoka kata za Msamalo, Ikoa na Igandu, hivyo ongezeko la huduma linahitaji miundombinu imara zaidi ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

Amefafanua kuwa kukamilika kwa majengo ya upasuaji na huduma za mama na mtoto kutasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa pamoja na kupunguza rufaa zisizo za lazima kwenda hospitali za mbali.

“Tunashukuru kwa hatua iliyofikiwa kupitia TASAF, lakini bado tunaiomba Serikali na wadau wa maendeleo kuhakikisha miundombinu iliyobaki inakamilishwa ili huduma ziwe bora zaidi,” alisema Kitundu.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ukaguzi wa Ndani, Uswege Edward akizungumza wakati wa ziara hiyo

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ukaguzi wa Ndani, Uswege Edward, aliipongeza Serikali kwa ushirikiano wake katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia TASAF, akisema umeleta mabadiliko chanya katika sekta mbalimbali ikiwemo afya.

Alibainisha kuwa awamu ya pili ya mpango huo imewezesha uboreshaji wa huduma za jamii katika maeneo mengi nchini, huku akishukuru pia wadau wa maendeleo wakiwemo Ubalozi wa Uswisi kwa kuendelea kufuatilia na kushirikiana katika miradi hiyo.

Aidha, aliwahimiza wananchi waliopitia katika mpango huo na kufikia hatua ya kujikwamua kiuchumi kuendelea kushiriki shughuli za uzalishaji mali ili kudumisha mafanikio yaliyopatikana kupitia programu hiyo ya kijamii.

Serikali imetangaza kuwa awamu ya tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia TASAF inatarajiwa kuanza kutekelezwa hivi karibuni katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayotarajiwa kuongeza wigo wa miradi ya maendeleo na kuimarisha zaidi huduma za msingi kwa wananchi, hususan katika sekta za afya, elimu na miundombinu ya kijamii.