Habari
Ridhiwani Kikwete avutiwa na miradi ya TASAF Simiyu

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe Ridhiwani Kikwete ameeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini TASAF Mkoani Simiyu.
Mhe. Kikwete amezitaka halmashauri nchini zinazotekeleza miradi ya maendeleo hususani kwenye sekta ya huduma za jamii kujifunza kutoka mkoa wa Simiyu ambao umeonesha mafanikio makubwa.
Naibu Waziri ameyasema hayo mjini Bariadi baada ya kupekea ripoti ya utelekezaji wa miradi ya TASAF katika mkoa wa Simiyu ambao pia miongoni mwa mikoa mitano inayotekeleza miradi ya kupunguza umasikini chini ya OPEC.
“Simiyu ni miongoni mwa mikoa ya mfano kwa utekelezaji na usimamizi mzuri wa miradi ya TASAF, nimeridhishwa sana na hatua kubwa iliyopigwa katika utelekezaji shughuli hizi ambazo zina lengo la kuondoa umasikini na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii,” alisema
Aidha, Mhe. Kikwete alisisitiza umuhimu wa waratibu na wasimamizi wa miradi ya TASAF kuendelea na ufuatiliaji wa karibu wakati wote wa utekelezaji kwa lengo la kuhakikisha thamani ya miradi yote inaendana na thamani ya fedha iliyotolewa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kikwete alisema serikali kupitia TASAF imesitisha uhawilishaji fedha kwa walengwa kwa njia ya mitandao ya simu kwa muda hadi hapo marekebisho ya kuondoa changamoto za kupokea fedha kwa njia hizo zitakapotatuliwa, na badala yake, zoezi hilo litafanyika kwa njia ya benki au mlengwa kupewa fedha mkononi.
“Kumekuwa na changamoto kadhaa kwenye uhawilishaji fedha kwa njia ya simu, sasa ili kuepukana na changamoto hizo kwa sasa, walengwa watapokea fedha hizo kwa njia ya benki au kuchukua moja kwa moja,” alisema Mhe Naibu Waziri.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya TASAF kwa niaba ya katibu Tawala wa Mkoa Prisca Kayombo, Mratibu wa TASAF mkoa Nyasilu Ndulu alisema jumla ya shilingi bilioni 9.24 zimepokelewa kwa ajili utekelezaji wa miradi hiyo ambayo ni zahanati 9, Nyumba 14, majengo ya wagonjwa wa nje (OPD) 2, jengo la upasuaji 1, jengo la kuhifadhia maiti 1, wodi za mama na mtoto 5 pamoja na maabara 1 na kwa sekta ya elimu fedha hizo zimewezesha kujengwa vyumba 60 vya madarasa, ofisi 27 za walimu, matundu ya vyoo 186, maktaba 1, nyumba za walimu 4, majengo ya utawala 4 vyumba vya maabara 8 na mabweni 11.