Habari
Awamu ya Tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kuanza hivi karibuni
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) unatarajia kuanza kutekeleza Awamu ya Tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mwezi Septemba mwaka huu, ukianza na kaya 575,000 mpya katika mamlaka 100 kati ya 186 za utekelezaji zilizopo Tanzania Bara na Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Shedrack Mziray, ameyasema hay oleo jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya maandalizi ya mpango huo mbele ya Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar iliyotembelea makao makuu ya taasisi hiyo.
Mziray amesema awamu hiyo mpya ipo hatua za mwisho za maandalizi na unatarajiwa kugharimu dola za kimarekani milioni 296, huku muundo wake ukizingatia vipaumbele vya taifa na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
Amesema katika hatua ya kwanza, utekelezaji utaanza katika mamlaka 100 kutokana na kiwango cha fedha kilichopatikana, huku maeneo yatakayohudumiwa yakichaguliwa kwa kuzingatia viwango vya umaskini na athari za mabadiliko ya tabianchi.
"Tunatarajia kuanza utekelezaji mwezi Septemba baada ya kukamilika kwa maandalizi muhimu," amesema Mziray.
Amesema tofauti na awamu zilizopita, walengwa wa awamu hiyo watakuwa kaya mpya ambazo hazikuwahi kunufaika na mpango wa kwanza na wa pili.
_1787040505.jpeg)
Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Machano Othman Said
Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Machano Othman Said, ameipongeza TASAF kwa kazi kubwa waliyofanya kwenye utekelezaji wa awamu zilizopita
Ameema mpango huo umechangia kuboresha maisha ya wananchi wengi kupitia ujenzi wa vituo vya afya, shule na kuwawezesha baadhi ya walengwa kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jimbo la Tumbe, Mmanga Mohammed Hamed, ameshauri walengwa watakaokuwa wamejikwamua kiuchumi waondolewe kwenye mpango huo ili nafasi zao zitolewe kwa kaya nyingine zenye uhitaji mkubwa zaidi.
Naye Mwakilishi Masoud Amour Masoud amesema TASAF imekuwa miongoni mwa programu muhimu zinazowasaidia wananchi maskini kuboresha maisha yao.
_1787040648.jpeg)
