Habari
TASAF yaimarisha uchumi wa kaya Ruvu Darajani,Uswisi yapongeza

Mkuu wa Idara ya Afrika katika Shirika la Maendeleo la Uswisi Nicolas Randin akiangalia mikeka inayofumwa na mmoja wa walenga wa TASAF
katika kujiingizia kipato cha kaya yake
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini umewezesha walengwa wa TASAF katika kijiji cha Ruvu Darajani kujikita katika shughuli mbalimbali za ujasiriamali na kujiunga katika vikundi vya kuweka na kukopa ambayo vinawasaidia katika kuongeza mitaji ya biashara zao zikiwa pamoja na kilimo na ufugaji
Sambamba na hayo, walengwa pia wamefanikiwa kufungua mawasiliano ya barabara katika vitongoji vinne katika kijiji hicho kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoa wa Pwani baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara mbili ambapo moja ina urefu wa kilomita 1.8 na nyingine yenye kilomita 1.5 katika vitongoji vya Mlimani, Mwenjeni, Relini na Mkwajuni kwa gharama ya shilingi milioni 26.8
Ujenzi wa barabara hizo umerahisiha mawasiliano baina ya vijiji na vitongoji jirani na kuimarisha uchumi wa walengwa umepongezwa na Serikali ya Uswisi ambao ni miongoni mwa wadau wa maendeleo wanaochangia fedha za utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Akizungumza katika ziara ya kuangalia maendeleo na shughuli wanazozifanya na walengwa katika kujiingizia kipato, Mkuu wa Idara ya Afrika katika Shirika la Maendeleo la Uswisi Nicolas Randin alisema wanaridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania kupitia TASAF katika kupunguza umasikini nchini.
Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Ruvu Darajani Asia Mayange alisema utekelezaji wa mpango wa TASAF umesaidia kuongeza mzunguko wa fedha pamoja na kuinua hali za maisha kwa walengwa.